Ufaransa: Video ya ngono yakatisha safari ya umeya ya mshirika wa rais Macron
by RFIVideo ya ngono iliyovuja kwenye mitandao ya kijamii ikimuhisisha mmoja wa wagombea wa nafasi ya umeya wa jiji la Paris kupitia chama tawala, Benjamin Griveaux ametangaza kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Benjamini ambaye aliwahi kuwa msemaji wa Serikali ya rais Emmanuel Macron, na ambaye alikuwa akiongoza katika kura za maoni kuwa meya wa jiji la Paris, amejikuta akilengwa na msanii wa Urusi aliyemtuhumu kwa ubinafsi.
Akizungumza na wanahabari, Griveaux, amesema hakuna mtu yeyote ambaye anatakiwa kudhalilishwa kwa namna iliyomtokea.
Video hiyo ambayo inamuonesha mwanaume mmoja akiwa katika hali ya utupu, ilisambaa kupitia mitandao ya kijamii siku ya Alhamisi.
Petr Pavlensky ambaye aliomba hifadhi nchini Ufaransa mwaka 2017, alithibitisha kuwa ndiye aliyechapisha video hiyo kwenye tovuti.
Namna gani Wafaransa walivyozungumzia mkasa huu
Wapinzani kutoka vyama mbalimbali nchini humo wamepaza sauti zao. Meya wa sasa Anne Hildalgo, ametoa wito kwa watu kuheshimu mambo binafsi ya watu, huku kiongozi wa mrengo wa kushoto Jean-Luc MĂ©lanchon akilaani kitendo hicho.
Kinara mwingine wa upinzani nchini humo, Marin Le Pen, yeye amenukuliwa akisema Griveaux pengine kwa misingi ya demokrasia hakupaswa kujiuzulu nafasi yake.
Waziri mkuu Edouard Philippe ameonesha kumuunga mkono rafiki yake wa zamani, huku waziri wa mambo ya ndani Christophe Castaner yeye akienda mbali Zaidi na kuonya watu dhidi ya kuchapisha mambo ambayo wahusika hawajaridhia yachapishwe na kwamba watakaoenda kinyume watakabiliwa na faini au kifungo cha miaka miwili jela.