Benki Kuu ya Burundi yaagiza kufungwa kwa maduka ya kubadilishia fedha
by RFIBenki kuu nchini Burundi, BRB, imetangaza kuyafunga maduka yote ya kubadilisha fedha kufIkia siku ya Jumamosi, kwa madai kuwa wamiliki wa maduka hayo wamekuwa wakifanya shughuli zao kinyume na utaratibu uliowekwa na Serikali, ni hatua ambayo itasababisha watu kukosa ajira.
Gavana wa Benki kuu nchini humo Jean Ciza, amesema uchunguzi wao umebaini kuwa tangu mwezi Septemba mwaka2019, maduka hayo ya kubadilishia fedha yamekuwa yakipuuza matakwa yaliyowekwa na benki hiyo.
“Maelekezo ni kuwa ofisi hizi za kubadilishia fedha sasa zinafungwa. Wamiliki Wake wanapaswa kuondoa mabango yote waliyoweka. Na sasa benki zote za kibiashara ndizo zitaruhusiwa kubadilisha fedha,” amesema Gavana Ciza.
Uamuzi huu umeonekana kuwashangaza na kuwachukiza wamiliki wa maduka hayo jijini Bujumbura, akiemo mmoja ambaye kwa sababu za kiusalama, hakutaka kufahamika lakini alituambia anachopitia.
“Unapohitaji pesa hizo kwenye beki yoyote hapa haupati! ukienda kwenye benki kuu ya nchi vilevile haupati! Kwa hivyo kwa serikali jinsi vile naona sio tu waseme wenye vituo waheshimishe viwango...na wakati hawajawapata hizo pesa au wawahudumie kwa kiwango wanachohitaji hapa.”
Wataalamu wa masuala ya uchumi wao wanaona kuwa hatua hiyo itaendelea kusababisha hali ngumu ya kiuchumi nchini Burundi.
“Uhaba wa pesa za kigeni itakuwa mojawapo ya shida za kiuchumi Burundi. Kumbuka vyanzo vya sarafu za kigeni vimekauka kutokana mzozo wa kisiasa katika nchi hiyo.Uwekezaji wa ndani pia umeporomoka kwa ukosefu wa utulivu,” amesema Henry Obwocha mtalaam wa masuala ya uchumi akiwa jijini Nairobi nchini Kenya.
Tangu kutokea kwa vurugu za baada ya uchaguzi mkuu uliopita, uchumi wa Burundi uchumi wa nchi hiyo ndogo ya Afrika ya Kati, umekuwa ukisuasua hali ambayo imeifanya sarafu ya Franka kupoteza thamani.