Marekani kusaidia kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona nchini Korea Kaskazini
by RFIMarekani imesema kuwa ina "wasiwasi" kuhusu athari inayowezekana ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona unaofahamika kwa jina la Covid-19 nchini Korea Kaskazini.
Washington iko tayari kuwezesha juhudi za mashirika ya Marekani na ya kimataifa kupambana na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo hatari nchini Korea Kaskazini, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imebaini.
"Tunaunga mkono sana na tunapongeza kazi ya mashirika ya kibinadamu ya Marekani na yale ya kimataifa na mashirika ya afya kukabiliana na kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Covid-19 nchini Korea Kaskazini," amesema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, baada ya Shirika la Msalaba Mwekundu kutoa wito wa Korea Kaskazini kupewa msamaha kwa vikwazo vinavyoikabli kwa kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo nchini humo.
"Marekani iko tayari kuwezesha haraka kutoa idhini ya misaada kutoka kwa mashirika haya," ameongeza Morgan Ortagus katika taarifa.
Mapema Shirikisho la kimataifa la Msalaba Mwekundu lilisema kwamba kuna mahitaji ya haraka ya vifaa vya ulinzi na ugunduzi ili kuzuia uwezekano wa mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 nchini Korea Kaskazini, inayopakana na China Bara ambapo ugonjwa huo ulianzia mwezi Desemba mwaka jana.
Hakuna kesi ya yoyote ya mambukizi ambayo imeripotiwa nchini Korea Kaskazini, ambayo imechukua hatua thabiti kwa watu walio na dalili zinazojulikana za virusi vya ugonjwa wa Covid-19 na imefuta safari za anga na reli na nchi jirani.