Maelfu yaendelea kutikisa jiji la Hong Kong, wanaharakati wataka demokrasia
by RFIMaelfu ya waandamanaji wanaopigania demokrasia jijini Hong Kong wameandamana mwishoni mwa wiki iliyopita kuadhimisha miezi 6 tangu kuanza kwa maandamano yao kushinikiza mabadiliko, huku wanaharakati viongozi wakiwaonya wanasiasa wanaouunga mkono utawala wa Beijing.
Maandamano ya hapo jana yanatajwa kuwa makubwa zaidi ukilinganisha na yale yaliyopita, huku waandaaji wakidai kuwa watu zaidi ya laki 8 walijitokeza barabarani kuonesha mshikamano.
Polisi kwenye mji huo ambao mara zote wamekuwa wakiripoti idadi ndogo ya waandamanaji, wamesema watu zaidi ya laki 1 na elfu 83 walishiriki maandamano hayo, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodi.
Maandamano haya ambayo yalipata kibali kutoka kwa polisi yamekuja ikiwa ni majuma kadhaa yamepita tangu wanaaharakati wa masuala ya demokrasia wapate ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Wengi wa waandamanaji, walionesha wazi hasira zao dhidi ya kiongozi wa eneo hilo Carrie Lam na utawala wa Beijing ambao wametupilia mbali uwezekano wa kupata suluhu.